Kwa mujibu wa kitengo cha kimataifa cha Shirika la Habari la Hawza, kwa kunukuu Shirika la Habari la Anadolu, Numan Kurtulmuş, Rais wa Bunge la Uturuki, katika ufunguzi wa Mkutano Mkuu wa 152 wa Umoja wa Mabunge uliofanyika Istanbul, alitangaza kuwa; uanachama wa Israel ndani ya Umoja wa Mataifa unapaswa kusimamishwa. Mkutano huu ulifanyika kwa ushiriki wa wawakilishi takriban kutoka nchi 155, marais wa mabunge 80, na karibu wawakilishi 800.
Alirejea hali ya mgogoro wa dunia na kusema kuwa; mfumo wa kimataifa umeingia katika kipindi kipya na kigumu, na kwamba kanuni za zamani zimepoteza ufanisi wake; kiasi kwamba “sheria ya msitu” imekuwa ikitawala mahusiano ya kimataifa.
Kurtulmuş alisisitiza kuwa; taasisi za kimataifa, hasa Umoja wa Mataifa, zimepoteza ufanisi wake na hazijaweza kusimamisha vita na migogoro, ikiwemo hali ya Ukanda wa Ghaza. Akitaja kuuawa kwa zaidi ya watu 75,000 hukk Ghaza (wengi wao wakiwa wanawake na watoto), aliitaja hali hiyo kuwa ni mfano wa kushindwa kwa mfumo wa dunia.
Aidha, alirejea migogoro ya kikanda ikiwemo mvutano kati ya Iran, Marekani na Israel, na akauliza ni taasisi ipi ya kimataifa inayoweza kusimamisha migogoro hii.
Kurtulmuş, akieleza kuwa mfumo wa dunia umeathiriwa na “ufisadi na kusambaratika”, alitoa wito wa juhudi za kuunda mfumo wa haki zaidi. Akinukuu kusimamishwa kwa uanachama wa South Africa katika kipindi cha ubaguzi wa rangi (Apartheid), alisisitiza kuwa; kama ilivyofanyika wakati huo, leo pia uanachama wa Israel unapaswa kusimamishwa kutokana na mienendo inayofanana dhidi ya Wapalestina.
Pia alikumbusha mfano wa mwitikio wa Ulaya dhidi ya kuibuka kwa mrengo wa kulia mkali nchini Austria na kusema: Ikiwa kuna nia, Jumuiya ya kimataifa inaweza kuzuia kutokea au kuendelea kwa hali kama hizi.
Kurtulmuş aliendelea kusisitiza umuhimu wa umoja kwa ajili ya kuhakikisha maslahi ya wanadamu wote, usawa wa nchi katika mamlaka, na kupambana na ukiukaji wa mamlaka ya nchi kama Palestine, Lebanon, Syria na nchi nyingine za eneo hilo.
Mwisho, alitoa wito wa kuundwa kwa mfumo mpya wa dunia unaotegemea uadilifu, haki na usawa, na akasisitiza kuwa; mabunge yana jukumu muhimu katika kufanikisha lengo hili.

Maoni yako